Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo latumwa Myanmar kuchunguza ukiukwaji wa haki

Jopo latumwa Myanmar kuchunguza ukiukwaji wa haki

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio kuhusu Myanmar ambalo pamoja na mambo mengine linaridhia kupelekwa kwa tume huru ya kimataifa nchini Myanmar ili kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo, hususan kwenye jimbo la Rakhine.

Wajumbe wa jopo hilo watachaguliwa na Rais wa Baraza hilo ambapo watachunguza madhila yanayoripotiwa kukumba wakazi wa jimbo hilo, madhila yanayodaiwa kutekelezwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya serikali pamoja na ukatili mwingine na manyanyaso.

Azimio hilo lililopitishwa bila kupigiwa kura, pia limeongeza kipindi cha mwaka mmoja zaidi kwa mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar.

Halikadhalika limetoa wito kwa serikali kuendelea na jitihada za kutokomeza mfumo wa baadhi ya watu kutokuwa na utaifi kwa misingi ya ubaguzi wa kikabila au dini hasa kwa jamii ya wachache ya Rohingya.