Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni mpya ya UM inatarajia kutokomeza Polio Afrika

Kampeni mpya ya UM inatarajia kutokomeza Polio Afrika

Kampeni ya chanjo ya aina yake kuwahi kufanyika katika bara la Afrika dhidi ya polio itatoa chanjo kwa watoto milioni 116 wiki ijayo katika nchi 13 za Afrika Magharibi na Kati limesema Shirika la Afya Duniani, WHO na Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

Kampeni hiyo ambayo itafanywa kwa wakati mmoja na wahudumu wakujitolea 190,000 kwa kutumia miguu, baiskeli na njia zingine zozote, ni katika harakati za kuutokomeza kabisa ugonjwa huo katika nchi zilizosalia waathirika, wa ugonjwa huo ambao WHO inasema bado ni tishio kubwa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5.

Mashirika hayo yamesema mapigano katika jimbo la Borno nchini Nigeria yalisababisha watoto wanne kupooza mwaka 2016 kutokana na ukosefu wa chanjo, eneo pekee ambalo kirusi cha Polio bado kinatishia maisha, na iwapo hakitashughulikiwa haraka, eneo hilo na maeneo yaliyojirani yatakuwa hatarini kuambukizwa.

Ili kufanikisha kampeni hiyo, mashirika hayo yamesema ushirikiano wa serikali kuu hadi za mashinani unahitajika ili kuweza kumfikia kila mtoto.

Nchi hizo 13 ni Benin, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Chad, Côte d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Guinea, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria na Sierra Leone.