Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano wa Baraza utumike kukwamua Somalia- Keating

Mshikamano wa Baraza utumike kukwamua Somalia- Keating

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha ngazi ya juu kuhusu Somalia ambapo wajumbe wameelezwa kuwa janga la kibinadamu nchini humo linaweza kuepukwa iwapo fedha zaidi zitakapatikana kukidhi mahitaji yanayotakiwa.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating amesema hali inazidi kuwa mbaya kwa kuwa hadi sasa ni asilimia 32 tu ya ombi la dola milioni 825 ndio zimepatikana wakati huu ambapo janga la ukame linatishia uhai wa wananchi zaidi ya milioni Sita.

Bwana Keating akaonyesha matumaini akisema..

(Sauti ya Keating)

“Baraza lina maafikiano ya kipekee kuhusu Somalia. Natumai kuwa maelewano hayo yanaweza kutumika kushughulikia hivi sasa janga linalokumba mamilioni ya wananchi, na pia kusaidia uongozi mpya wa Somalia, Rais mpya na Waziri Mkuu mpya kushughulikia vyanzo vitakavyozuia majanga kutokea tena.”

Bwana Keating ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia alitumia kikao hicho kuzungumzia suala la kuwezesha serikali mpya kuwa na mipango endelevu ya maendeleo akisisitiza suala la kukusanya kodi na kuvutia uwekezaji.

(Sauti ya Keating)

“Kama Somalia haitaanza kuvutia vitegauchumi vya dhati na kujipatia mapato ya ndani, ujenzi wa nchi utasalia ndoto na nchi hiyo itaendelea kuwa tegemezi na kuwa hatarini kuathiriwa na majanga.”