Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 20 zahitajika kusaidia wahanga wa kimbunga Enawo, Madagascar

Dola milioni 20 zahitajika kusaidia wahanga wa kimbunga Enawo, Madagascar

Umoja wa Mataifa na wadau wake wametoa ombi la dola milioni 20 ili kukabiliana na athari za kimbunga Enawo kilichopiga Madascar mapema mwezi huu.

Kimbunga hicho kikiambatana na upepo mkali na mvua iliyosababisha mafuriko, kilipiga maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo na sasa watu takribani laki mbili na nusu wanahitaji misaada ya dharura kuokoa maisha yao.

Tayari serikali imetangaza hali ya dharura ikieleza kuwa asilimia 85 ya mazao yaliyokuwa yamepandwa yamesombwa, visima vya maji vimechafuliwa, vituo vya afya zaidi ya 100 na madarasa 3,300 yamebomolewa.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Madagascar Violet Kakyoma amepongeza serikali kwa hatua zake za kuhamisha wananchi kabla kimbunga hakijatua akisema sasa wanashirikiana na mamlaka husika kukidhi mahitaji.

Amesema fedha zinazoombwa pamoja na mambo mengine zitawezesha kuwapatia chakula watu 170,00 na kusaidia wakulima kupanda upya mazao yao, wafugaji kusaka mifugo na kaya 20,000 zilizopoteza nyumba zao kupata makazi ya muda.