Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada kwa wakimbizi wa Sudan kusini wahitajika haraka-UNHCR/Uganda

Msaada kwa wakimbizi wa Sudan kusini wahitajika haraka-UNHCR/Uganda

Serikali ya Uganda na kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR,  Filippo Grandi  leo Alhamisi wametoa ombi la pamoja kwa jumuiya ya kimataifa kutoa haraka msaada kwa maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoendelea kuwasili Uganda kila siku  wakikimbia vita na sasa uhaba wa chakula. Taarifa kamili na Rosemary Musumba.

(Taarifa ya Rosemary)

Uganda hivi sasa inahifadhi wakimbizi zaidi ya laki nane wa Sudan Kusini , na miongoni mwao wakimbizi wapya 572,000 waliowasili Uganda wakihitaji usalama na msaada tangu Julai 8 mwaka 2016.

UNHCR inasema kwa kiwango cha sasa cha wakimbizi wanaoingia kila siku idadi hiyo itazidi milioni moja kabla ya katikati ya mwaka huu. Kwa mujibu wa waziri mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda Uganda inaendelea kufungua mipaka yake lakini inahitaji msaada.

Naye Bwana Grandi amesema Uganda  sasa imefikia pabaya, peke yake haiwezi kukabili mgogoro mkubwa kabisa wa wakimbizi Afrika, na ukosefu wa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa kwa watu wanaoteseka wa Sudan kusini ni kuwaangusha hasa katika wakati huu wanaohitaji zaidi msaada.