Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa muongozo wa maadili ya kulinda haki za wagonjwa wa kifua kikuu

WHO yatoa muongozo wa maadili ya kulinda haki za wagonjwa wa kifua kikuu

Muongozo mpya wa maadili kwa ajili ya kulinda haki za wagonjwa wa kifua kikuu au TB umezinduliwa leo Jumatano na shirika la afya ulimwenguni WHO , ukiwa na lengo la kusaidia kuhakikisha kwamba nchi zinatekeleza mkakati wa kutokomeza TB zikizingatia maadili ya kuwalinda wote walioathirika na maradhi hayo.

Kifua kikuu moja ya maradhi makubwa ya kuambukiza na kuua, hukatili maisha ya watu 5000 kila siku na mzigo mkubwa wa gonjwa hilo hubebwa na wale ambao tayari wana changamoto za kijamii na kiuchumi kama wahamiaji, wakimbizi, wafungwa, jamii za walio wachache,wachimba migodi na wengine wanaofanya kazi na kuishi katika mazingira ya hatari, pia makundi yanayotengwa kama wanawake, watoto na wazee.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret Chan , shirika hilo limejidhatiti kukabiliana na unyanyapaa, ubaguzi na vikwazo vingine ambavyo huzuia watu wengi kupata huduma wanazozihitaji. Ameongeza kuwa zaidi ya watu milioni 4.3 wenye TB hawapiwmi au hawaripotiwi, na wengine hawapati kabisa tiba au huduma inayostahili.

Muongozo mpya shirika hilo linasema utashughulikia masuala kama kutengwa kwa wagonjwa wa kuambukiza, haki ya waginjwa wa kifua kikuu magerezani, sera za kibaguzi dhidi ya wahamiaji walioambukizwa TB miongoni mwa mambo mengine na unasisitiza masuala matano ya kimaadili ambayo ni wajibu wa serikali, wahudumu wa afya, watoa huduma, asasi za kiraia, watafiti na wadau wengine ambayo ni : Mosi kutoa msaada wa kijamii unaohitajika na wagonjwa ili waweze kutimiza majukumu yao, pili kujizuia kuwatenga wagonjwa wa TB kabla ya kuangalia njia zote za matitabu, tatu kuruhusu wahamiaji kupata fursa ya huduma za afya zinazotolewa kwa raia , nne kuhakikisha wahudumu wa afya wanafanya kazi katika mazingira salama na tano kushirikiana matokeo ya utafiti ili kutoa taarifa zitakazotumika katika sera za kitaifa na kimataifa za TB.