Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majitaka ni mweleko mpya wa kukabili uhaba wa maji- WHO

Majitaka ni mweleko mpya wa kukabili uhaba wa maji- WHO

Leo ni siku ya maji duniani ambapo shirika la afya ulimwenguni, WHO linasem majitaka yanaweza kuwa suluhu ya uhaba wa maji unaokabili binadamu hivi sasa. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Itakuwa vipi tukibonga bongo kuhusu matumizi bora ya majitaka kutoka majumbani, mashambani na viwandani, majitaka yanayoelekezwa katika mazingira kila uchao?

Hivyo ndivyo ripoti ya WHO kuhusu siku ya maji duniani inahoji watunga sera ili wabadili mtazamo kwani maji hayo yana madini na virutubisho vya kutosha kukuza mimea.

Ripoti inasema nchi tajiri ndio angalau zinatumia upya majitaka ilhali kwa nchi maskini ni asilimia 8 tu hali inayofanya majitaka kuenea na kusambaza magonjwa badala ya kutumika upya hata na binadamu iwapo yanawekewa dawa.

Stefan Uhlenbrook kutoka taasisi ya Umoja wa Mataifa iliyoandaa ripoti hiyo anasema bado watu wengi wanateswa na kinyaa, kuwa iweje majitaka yananywewa, lakini anasema.

(Sauti ya Stefan)

"Miji kama San Diego au Singapore hufanya hivyo kila wakati, wanaweka dawa kwenye majitaka na yanakuwa ya kunywa. Kuna teknolojia, hivyo wanaelimisha umma kuwa ni salama kunywa, ili kuondoa kile kinyaa kuwa unakunywa maji taka. Hivyo Singapore wanayaita ni maji mapya na hiyo inakuwa bora kuliko kusema majitaka.”