Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yamuongezea Bemba mwaka mmoja jela kwa rushwa

ICC yamuongezea Bemba mwaka mmoja jela kwa rushwa

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague Uholanzi imemuongezea Jean-Pierre Bemba hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la rushwa. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora)

Bemba ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ameongezewa kifungo hicho wakati huu ambapo tayari anatumikia kifungo cha miaka 18 jela kwa makosa ya uhalifu wa kivita aliyotekeleza huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Jaji Bertram Schmitt wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague Uholanzi ametoa hukumu hiyo leo dhidi ya Bemba pamoja na mawakili wake wanne wa upande wa utetezi.

Halikadhalika Bemba anatakiwa kulipa faini ya zaidi ya dola laki tatu lengo ni kuhakikisha vitendo kama hivyo havirudiwi tena.

Fadi El Abdallah ni msemaji wa ICC

(Sauti ya Fadi)

“Kuingilia ushahidi wa ICC na vitendo vya kukwamisha haki ni uingiliaji mkubwa ambao unaadhibiwa kwa mujibu wa mkataba wa Roma.”