Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikosi cha kikanda kuwasili Sudan Kusini- Ladsous

Kikosi cha kikanda kuwasili Sudan Kusini- Ladsous

Umoja wa Mataifa umesema kuwa kikosi cha kikanda cha ulinzi kitaanza kuwasili Sudan Kusini wiki chache zijazo, ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la umoja huo.

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous amesema hayo leo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini alikokuweko ziarani kwa siku mbili baada ya ziara kama hiyo nchini Mali.

Amewaambia waandishi wa habari kuwa upelekaji wa kikosi hicho umechelewa kutokana na kuchelewa kwa vibali lakini sasa kila juhudi zinafanyika ili kikosi cha kwanza kiwasili na watendaji watatoka Rwanda, Nepal, Bangladesh na Ethiopia.

(Sauti ya Ladsous)

Sasa tunaharakisha kuleta kikosi cha ulinzi cha kikanda . Tulipoteza muda kwa sababu ya kusuasua kwa vibali lakini sasa hatupotezi tena muda. Na nadhani naweza kusema kuwa wiki chache zijazo utaona kikosi cha kwanza kikiwasili, na bila shaka hapa Juba. Na hiyo nadhani itakuwa ni muhimu sana ili kuashiria kuwa mambo yanasonga.”

Mwezi Agosti mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kikosi cha kikanda cha askari 4,000 huko Sudan Kusini ili kukabiliana na ongezeko la ghasia.

Awali Bwana Ladsous alikutana na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ambapo walijadili changamoto zinazokabili wafanyakazi wa kibinadamu nchini humo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa operesheni za ulinzi wa amani, Sudan Kusini ni nchi yenye visa vingi vya wafanyakazi wa kibinadamu kuzuia kufanya kazi yao.