Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvutano wa nani awe Waziri Mkuu DRC ndio kikwazo- Ripoti

Mvutano wa nani awe Waziri Mkuu DRC ndio kikwazo- Ripoti

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, bado umekwama, ikiwa ni miwili tangu yatiwe saini.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, kuhusu DRC, ripoti iliyowasilishwa na mwakilishi wake maalum nchini DRC, Maman Sambo Sidikou.

(Sauti ya Maman)

“Baadhi ya vikwazo vimeibuka na lazima viondolewe miongoni mwa wengi walio madarakani na upinzani juu ya uteuzi wa Waziri Mkuu na mgao wa wizara nyeti kama ile ya mambo ya nje, ndani na sheria katika serikali ya mpito.”

Akijibu hoja ya kucheleweshwa kwa uteuzi wa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa kikanda wa DRC Leonard She Okitundu amesema serikali haina nia ya kufanay hivyo na badala yake ametoa wito kwa upinzani hasa jumuiko la wapinzani wamalize tofauti zao za uteuzi ambazo zimeibuka baada ya kifo cha Etienne Tshisekedi.

(Sauti ya Leonard)

“Serikali inataka kuhakikishia baraza kuwa haina nia yoyote ya kuchelewesha utekelezaji wa mkataba, na ucheleweshaji wowote unatokana na hali halisi ikiwemo kufariki dunia kwa Tshisekedi, kifo kilichosababisha CENCO kusitisha shughuli zake. Tunaamini kuwa kwa kuanza tena kwa mashauriano tarehe 16 mwezi huu, pande husika zitaweza kupata suluhu ya mambo wanayokinzana.”