Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baadhi ya nchi mke anahitaji kibali cha mume kufanya kazi- Ripoti

Baadhi ya nchi mke anahitaji kibali cha mume kufanya kazi- Ripoti

Ripoti mpya ya maendeleo ya binadamu duniani kwa mwaka 2016 imezinduliwa huko Stockholm, Sweden ikionyesha kuwa katika miaka 25 iliyopita kumekuwepo na mafanikio licha ya changamoto za baadhi ya watu kuendelea kuenguliwa.

Nats..

Uzinduzi wa nyaraka hiyo iitwayo "Ripoti ya maendeleo ya binadamu na nani ameachwa nyuma?" huo ulienda sambamba na uonyeshwaji wa video kuhusu ripoti hiyo ikitaja mafanikio kuwa ni pamoja na kupungua kwa umaskini na njaa, kupungua kwa idadi ya vifo, teknolojia kushika kasi, ushiriki wa watu kwenye masuala yanayowahusu kuongezeka pamoja na kuimarika kwa hudum za kiafya na kijamii.

Hata hivyo changamoto zilizokwamisha maendeleo kuenea katika nchi zote zimeendelea kuwepo kama anavyosema kiongozi mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, Helen Clark wakati wa uzinduzi huo.

(Sauti ya Helen)

"Kuna nchi ambako kibali cha mume kinahitajika ili mwanamke aweze kufanya kazi. Na katika takribani nchi 100 wanawake wananyimwa haki ya kufanya baadhi ya kazi kwa sababu ni wanawake.”

Hivyo amesema ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kila mtu..

(Sauti ya Helen) 

“Kutahitaji tuwe na takwimu sahihi na uchambuzi bora ili kutekeleza sera na kuchukua hatua. Mifumo ya takwimu ya kitaifa inapaswa kukusanya takwimu hizo kwa kuzingatia vigezo vyenye wigo mpana zaidi vya kijamii. Hata takwimu kwa misingi ya jinsia bado hazijitoshelezi katika nchi nyingi.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Norway inaongoza kwa kiwango cha maendeleo duniani, huku kwa nchi za Afrika Mashariki Kenya ni ya 145, Tanzania ya 151 ilhali Uganda na Rwanda zimefungana nafasi ya 163, Sudan Kusini ya 169 na Burundi ni ya 184.