Ubaguzi na ghasia kwa misingi ya rangi vinaongezeka-Guterres

21 Machi 2017

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres amesema siku ya leo ya kutokomeza ubaguzi wa rangi inakumbusha machungu ya mwaka 1960 nchini Afrika Kusini ambapo waandamanaji 69 waliuawa kwa misingi ya kibaguzi wakati wa uatawala wa makaburu, lakini miaka 57 baadaye inaonekana dunia ipo katika ongezeko la hali ya kutovumiliana na mgawanyiko mkubwa, huku ubaguzi na ghasia vikiongezeka. Grace Kaneiya na taarifa zaidi

(TAARIFA YA GRACE)

Katika ujumbe maalumu wa siku hii Guterres amesema watu wanalengwa kwa sababu ya rangi yao, utaifa wao, kabila lao, dini au mtazamo wao wa kimapenzi, chuki dhidi ya wageni ikiongezeka na imani ikipungua. Ameongeza kuwa mipaka inafungwa na ulinzi kwa wakimbizi na wahamiaji uko matatani.Hata hivyo anasema kuna matumaini.

(SAUTI YA GUTERRES)

“ Mara nyingi hotuba za chuki , kuwatenga watu na unyanyapaa vinakuwa vitu vya kawaida. Wakiukaji haki wamechukua nafasi ya juu, na licha ya taswira hii ya kiza kuna mwangaza wa matumaini. Mamilioni ya watu sasa wanazungumza kupinga ubaguzi wa rangi na kutovumiliana.”

Amesisitiza kuwa siku ya leo ni ya kuahidi kuendeleza juhudi hizo na kufanya kazi ya ziada kuziba pengo la mgawanyiko, kumaliza hali ya kutovumiliana na kuchagiza haki za binadamu kwa wote , akizitaka nchi zote kuungana katika kampeni ya kimataifa ya kulinda, kuheshimu usalama na utu kwa wote.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud