Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wazindua kituo cha kuratibu misaada ya kibinadamu Somalia

Umoja wa Mataifa wazindua kituo cha kuratibu misaada ya kibinadamu Somalia

Nchini Somalia, Umoja wa Mataifa umezinduzia kituo cha kuratibu operesheni za kukabiliana na ukame ikiwemo usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa ufanisi hususan kusini magharibi mwa nchi.

Naibu mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Vincent Lelei amesema kituo hicho kipo kwenye mji wa Baidoa na kitakuwa ni muhimu wakati huu ambapo watu takribani 2,000 kwenye jimbo la Kusini-Magharibi wanaugua kipindupindu na watoto wengi wana utapiamlo.

(Sauti ya Vincent)

“Janga la kibinadamu kwenye jimbo la Kusini-Magharibi hasa kwenye maeneo ya Bay, Bakool na Shabelle chini limekuwa baya zaidi kuliko maeneo yote Somalia. Matokeo yake tumefungua kituo kipya cha uratibu kuhakikisha tunafikia wale wote wanaohitaji misaada. Hicho ni kipaumbele cha kwanza! Na kipaumbele cha pili ni kufanya kazi na maafisa wa jimbo na wilaya kuhakikisha mpango wetu una tija.”

Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni sita nchini Somalia, idadi ambayo ni nusu ay wakazi wa nchi hiyo wanahitaji msaada wa kibinadamu.