Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watoto milioni 600 wataishi kwenye uhaba wa maji ifikapo 2040-UM

Takriban watoto milioni 600 wataishi kwenye uhaba wa maji ifikapo 2040-UM

Takriban watoto milioni 600 au 1 kati ya 4 kote duniani wataishi katika maeneo ambayo yana uhaba mkubwa wa maji ifikapo mwaka 2040 kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto  UNICEF iliyotolewa Jumatano  katika siku ya maji duniani.

Ripoti hiyo ‘kiu kwa siku za usoni:maji na watoto katika mabadiliko ya tabia nchi” inaangalia vitisho kwa maisha ya watoto na mustakhbali wao vinavyosababishwa na kupungua kwa rasilimali ya maji na njia ambazo mabadiliko ya tabia nchi yanazidisha hatari hiyo katika miaka ijayo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa UNICEF Anthony Lake, maji ni muhimu sana na bila maji hakuna kitakachoota. Lakini duniani kote mamilioni ya watoto hawana fursa ya maji salama, hali inayoweka maisha yao hatarini , afya yao mashakani na mustakhbali wao njia panda .

Ripoti hiyo inasema nchi 36 duniani hivi sasa zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji . Miongoni mwa nchi hizo ni Sudan Kusini. Atokako salva Dut mwanzilishi wa mradi wa maji kwa ajili ya Sudan Kusini (WFSS) wenye lengo la kuwapunguzia adha ya kwenda kuteka maji hususani wanawake na wasichana

(SAUTI YA SALVA DUT)

“fursa ya watu Sudan Kusini kupata maji ni ngumu sana, na sasa ni ngumu hata zaidi sababu ya vita tulivyonavyo, wanawake na wasichana ndio muhimuli wa uchumi, na wao ndio wanaolazimika kutembea maili na maili kutafuta maji kila siku na sasa kuwa na kisima karibu nao hawatumii tena muda mrefu kutembea , wana muda wa ziada kupika lishe bora na kufanya mvitu vingine kwa ajili ya familia kama miradi midogomidogo”

Kwa ujumla watu hadi milioni 663 kote duniani hawana fursa ya kupata maji ya kutosha na milioni 946 hawana vyoo wanajisaidia haja kubwa kwenye maeneo ya wazi.