Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatari ya hotuba za chuki inaongezeka-Zeid

Hatari ya hotuba za chuki inaongezeka-Zeid

Kila mmoja anahitaji kuongeza juhudi katika kukabiliana na ubaguzi wa rangi, hotuba za chuki na uhalifu wa misingi ya kikabila. Huo ni ujumbe wa Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, katika kuelekea siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi ambayo kila mwaka huadhimishwa Machi 21.

Zeid amesema hatari ya watu kuchukiwa kutokana na rangi ya ngozi zao, taifa au dini ni dhahiri duniani kote. Katika ujumbe huo amegusia machafuko ya chuki dhidi ya wageni na ghasia dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini.

Ameongeza kuwa Sudan Kusini hotuba za chuki zimeliingiza taifa hilo changa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe karibu nchi nzima, wakati huko Myanmar, Waislam wa kabila la Rohingya wanateseka na ukiukwaji mkubwa wa haki zao, ukiambatana na ripoti za mauaji, ya watoto na ubakaji.

Zeid amemtaka kila mmoja kupambana na lugha za hofu na uchukivu, kwani amesema zina madhara makubwa sana, akitolea mfano ongezeko la uhalifu utokanao na chuki baada ya kura ya maoni ya Uingereza kujiondoa Muungano wa Ulaya, au ongezeko la asilimia 42 la mashambulizi dhidi ya wakimbizi na wahamiaji nchini Ujerumani.

Amezitolea wito nchi kuanza kukusanya takwimu za uhalifu utokanao na chuki, akizikumbusha kwamba zina wajibu wa kukomesha ubaguzi kwa kupitisha sheria zinaouharamisha.