Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya udogo, smurfs wapigia chepuo malengo makubwa ya SDGs

Licha ya udogo, smurfs wapigia chepuo malengo makubwa ya SDGs

Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa vikaragosi vya filamu ya Smurfs: The Lost Village wameadhimisha siku ya furaha duniani kwa kuungana na Umoja wa Mataifa kuchagiza kampeni ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Ikipatiwa jina Smurfs wadogo na malengo makubwa, kampeni hiyo inalenga kuhamasisha vijana popote pale walipo kujifunza kuhusu malengo 17 ya SDGs na kusaidia katika kufanikisha kutekeleza ili hatimaye dunia iwe pahala pema pa amani, usawa na afya.

Smurfs wametumia fursa ya leo kutambua vijana watoto ambao wamechukua hatua kusongesha SDGs na vijana hao ni Karan Jerath, Sarina Divan na Noor Samee.

Mathalani, Karan yeye amegundua kifaa cha kuzuia mafuta machafu yaliyomwagwa kando mwa bahari na hivyo kulinda viumbe vya baharini huku Divan amechagiza harakati za UNWomen za kulinda watoto wa kike kwenye shule yake na Noor anaendesha blogu ya UNICEF inayosongesha masuala ya haki za kijamii.

image
Waliotia sauti kwenye filamu ya vikaragosi ya Smurfs. Kutoka kushoto Mandy Patikins, Demi Lavato na Joe Manganiello, wakiwa katika hafla ya kusherehekea siku ya furaha duniani kwenye makao makuu ya UM jijini New York Marekani hii leo. (Picha: UNNews/Mustafa Al Gamal)
Vijana hao walipatiwa mfano wa ufunguo kama ishara ya kuwaruhusu kuingia katika kijiji cha Smurfs kilichomo kwenye filamu yao.

Akizungumza kwenye tukio hilo, mkuu wa idara ya mawasiliano kwa umma ya Umoja wa Mataifa Cristina Gallach amesema smurfs ingawa ni wadogo wameonyesha ni jinsi gani wanaweza kuweka mazingira bora kwa wao kuweza kuishi kwa amani na kwa furahi, hivyo akasema..

(Sauti ya Cristina)

“Na hili ni fundisho kuwa ni jambo muhimu sana kwetu sote, kila mmoja wao anamfundisha mwenzake na kila mmoja wetu awajibike kwa suala hilo na tunaweza kufanikisha mambo makubwa.”

Mwimbaji mashuhuri Demi Lovato ambaye ametia sauti ya Smurfette kwenye filamu ya vikaragosi hao akaunga mkono hoja ya Bi. Gallach.

(Sauti ya Demi)

"Smurfette ni mfano mzuri kwa jambo hilo kwa kuwa anaonyesha kuwa bila kujali u mdogo kiasi gani katika dunia hii unaweza kuleta tofauti kubwa.”

Ingawa Smurfs wamesherehekea siku ya furaha hii leo, duniani siku hii itaadhimishwa tarehe 20 mwezi huu wa Machi.

Mandy Patinkin ambaye amecheza kama baba kwenye familia hiyo ametaka vijana watumie fursa hiyo kusaidia hata wakimbizi ambao wanaishi katika mazingira magumu na hivyo kila mmoja achukue hatua na kila mkazi wa dunia awe na furaha.