Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ijapokuwa hali ya usalama bado ni tete CAR, maendeleo makubwa yamepatikana-Onanga

Ijapokuwa hali ya usalama bado ni tete CAR, maendeleo makubwa yamepatikana-Onanga

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA, Parfait Onanga-Anyanga, amesema japokuwa hali ya usalama bado ni tete, lakini maendeleo makubwa yamepatikana tangu tangu uchaguzi wa serikali mpya mapema mwaka jana. Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, Bwana Onanga-Anyanga amesema..

(Sauti ya Onanga-Anyanga)

"Tukilinganisha hali nchini CAR ilivyokuwa wakati ujumbe wa MINUSCA ulipoanza na mwaka mmoja uliopita Rais Toudera alipochaguliwa na sasa hivi, tumepiga hatua kubwa, Bangui ni tulivu na tunahisi kuwa vikundi vya waasi vyenye silaha vimeitikia wito wa Rais wa kuingia kwenye mpango wa kukabidhi silaha zao (DDR). "

Bwana Onanga-Anyanga yuko hapa katika makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New York na ametoa wito kwa nchi wanachama kuheshimu ahadi walizotoa za msaada wa dola bilioni 2.2 kwa CAR, katika mkutano maalum wa ufadhili uliofanywa Novemba mwaka jana.

Akizungumzia kuhusu MINUSCA na sababu ya kwa nini ilibidi ujumbe wake kutumia nguvu katika kupambana na vikundi vya waasi karibu na mji wa Bambari mwezi uliopita, ambapo askari wa kulinda amani wanne walijeruhiwa mwakilishi huyo amesema usalama wa raia ni muhimu na kama haingefanyika hivyo raia wengi wangeathirika na ameongeza kuwa ...

(Sauti ya Onanga-Anyanga)

"Leo ninafurahi kusema tulichokuwa tunasubiri kwa muda mrefu vikundi hivyo vya waasi karibu 14 vinavyojulikana wamekubali mwaliko wa Rais wa kuingia kwenye kamati ya kitaifa ya DDR na mkutano wao wa kwanza utafanyika Machi 23 ambapo yote yatazungumziwa ikiwemo chanzo cha mgogoro na hii ni ishara nzuri sana."

Mapigano kati ya waasi waislamu wa Seleka na wanamgambo wa Balaka ambao ni wakristo, yameitumbukiza nchi hiyo ya watu milioni 4.5 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013.