Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la wakimbizi wa Sudan Kusini laongezeka, msaada wahitajika-UNHCR

Janga la wakimbizi wa Sudan Kusini laongezeka, msaada wahitajika-UNHCR

Miezi minane baada ya kuzuka upya machafuko Sudan Kusini , baa la njaa lililosababishwa na mchanganyiko wa vita na ukame sasa limefanya janga la wakimbizi nchini humo kuwa moja ya mgogoro wa wakimbizi unaokuwa haraka duniani. Flora Nducha na taarifa kamili.

(TAARIFA YA FLORA)

Kwa mujibu wa shirik la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR watu waliotawanywa Sudan Kusini na kuingia katika nchi jirani ni milioni 1.6 huku kiwango kipya cha wakimbizi kikitia hofu. Shirika hilo linasema hakuna nchi ya jirani iliyo na kinga kwani wakimbizi wanaingia, Uganda, Sudan, Ethiopia, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), sasa mataifa hayo ambayo pia yana matatizo yake yanasema yamezidiwa na yanahitaji msaada ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi hao.

Babar Baloch ni msemaji wa UNHCR

(SAUTI YA BABAR BALOCH)

"Kufikia sasa ufadhili kwa ajili ya wakimbizi wa Sudan Kusini katika eneo zima ni asilimia 8 tu kutoka kiwango kinachohitajika cha dola milioni 781 za kimarekani, ombi la UNHCR kwa ufadhili wa Uganda una pengo la zaidi ya robo bilioni za kimarekani."