Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanafunzi Sudan Kusini wasindikizwa na polisi kufanya mitihani- UNMISS

Wanafunzi Sudan Kusini wasindikizwa na polisi kufanya mitihani- UNMISS

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS unawapatia wanafunzi wa kidato cha nne ulinzi wa polisi wanapokwenda kufanya mitihani yao ya mwisho wakati huu ambapo wanafunzi hao walikumbwa na hofu ya usalama.

Msemaji wa UNMISS, Daniel Dicknson ameiambia Radio Miraya ya Umoja wa Mataifa kuwa wanafunzi hao ni wale waliopo kwenye kituo cha hifadhi ya wakimbizi wa ndani huko Jebel, kilichopo mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na wamekuwa wakisindikizwa kwa wiki moja sasa.

(Sauti ya Daniel)

“Wanafunzi hao wanapanda mabasi na kusindikizwa na polisi wa Umoja wa Mataifa kutoka kituo cha hifadhi cha Jebel hadi kituo cha mitihani cha shule ya Gulu. Mchakato huu unaendelea vizuri sana na wanafunzi wameweza kufanya mitihani yao katika mazingira salama.”

Mchakato huu wa usafiri umewezeshwa kwa ushirikiano kati ya UNMISS inayotoa polisi na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo linatoa usafiri wa mabasi.

UNMISS imesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa watoto wa Sudan Kusini ndio msingi wa mustakhbali wa taifa hilo.