Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi Mkuu wa IOM alaani shambulio dhidi ya msafara wa wahudumu wa kibinadamu Sudan Kusini

Mkurugenzi Mkuu wa IOM alaani shambulio dhidi ya msafara wa wahudumu wa kibinadamu Sudan Kusini

Mkurugeni mkuu wa shirika la kimataifa la uhamiaji IOM William Lacy Swing,  hivi leo amelaani shambulizi dhidi ya msafara wa wafanyi kazi wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini liotokea Machi 14 na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine watatu kujeruhiwa. Wafanyi kazi hao walivamiwa na watu wenye silaha wasiojulikana walipokuwa  wanarudi Yirol Mashariki mwa Sudan Kusini baada ya operesheni za kibinadamu za kuokoa maisha kutokana na mlipuko wa kipindu pindu katika eneo hilo.

Bwana Swing amesema shambulizi hilo baya kwa wafanyakazi wa misaada na raia ni la kusikitisha na limefanyika katika eneo la Sudan Kusini lililo na haja kubwa ya msaada. Ameongeza kuwa nchi hiyo imezidiwa na ukosefu mkubwa wa mahitaji ya msingi kutokana na vita, baa la njaa na milipuko ya magonjwa na mashambulizi haya yanapunguza uwezo wa washirika wa kibinadamu kutoa msaada kwa mamilioni ya watu wanaouhitaji.

Timu ya maafisa 12 wa IOM wa huduma za afya, maji safi, na usafi wa mazingira (WASH) wamekuwa katika eneo la Yirol Mashariki tangu Februari 17 kutoa msaada kwa jamii zilizoathirika na mlipuko wa kipindupindu ulioanza mapema mwezi Februari, na tayari kuna visa vya zaidi ya watu 300 na vifo vya watu 10 vilivyoripotiwa .

Maafisa hao wamefungua vitengo vinne vya matibabu ya kipindupindu katika mi wa Yirol mashariki na kufanya ukarabati wa visima, kuhamasisha usafi na usambazaji wa vifaa vya usafi, ikiwa ni pamoja na tembe za kusafisha maji na hadi sasa tayari wamewafikia zaidi ya watu 25,000.