Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres azungumzia mapendekezo ya bajeti ya Marekani 2018

Guterres azungumzia mapendekezo ya bajeti ya Marekani 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ameazimia kufanyia marekebisho chombo hicho na kuhakikisha kuwa kinakidhi malengo na kuleta matokeo bora kwa gharama yenye unafuu.

Bwana Guterres amesema hayo kufuatia Ikulu ya Marekani kuweka wazi mapendekezo ya bajeti ya nchi hiyo kwa mwaka wa 2018, mapendekezo ambayo inaelezwa yanalenga kupunguza matumizi kwenye maeneo kadhaa ikiwemo ushirikiano wa kimataifa na kuongeza pesa kwenye matumizi ya kijeshi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari amemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa punguzo lolote la bajeti kwa Umoja wa Mataifa..

(Sauti ya Dujarric)

“Linaweza kushinikiza kupitishwa kwa hatua za muda ambazo zinaweza kukandamiza athari za muda mrefu za jitihada za marekebisho. Katibu Mkuu yuko tayari kujadili na Marekani na mwanachana yoyote yule jinsi ya kuweka mazingira bora ya kuwa na shirika lenye gharama nafuu ili kufanikisha malengo yetu ya pamoja.”

Kuhusu suala la kukabiliana na ugaidi Katibu Mkuu amenukuliwa akisema kuwa..

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu anakubaliana kabisa na umuhimu wa kutokomeza ugaidi lakini anaamini kuwa hili linahitaji zaidi ya matumizi makubwa kijeshi. Kuna umuhimu wa kushughulikia vichochezi vya ugaidi kwa kuendelea kuwekeza katika kuzuia mizozo, misimamo mikali, ulinzi wa amani, maendeleo endelevu na shirikishi, kuheshimu haki za binadamu na kushughuliki majanga ya binadamu kwa wakati muafkaka.”

Katibu Mkuu amesema jamii ya kimataifa inakabiliwa na changamoto kubwa duniani ambazo zinaweza kushughulikiwa kupitia mfumo thabiti wa kimataifa ambao kwao Umoja wa Mataifa unasalia kuwa ndio msingi.