Skip to main content

Mahakama ya haki kwa Sudan Kusini ni muhimu zaidi hivi sasa- Mogae

Mahakama ya haki kwa Sudan Kusini ni muhimu zaidi hivi sasa- Mogae

Mwenyekiti wa tume ya pamoja ya ufuatiliaji na tathmini ya hali ya Sudan Kusini, JMEC, Festus Mogae ameshutumu vikali ghasia, mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu unaotekelezwana vikundi vyote vilivyojihami nchini humo.

Akifungua mkutano wa wazi wa JMEC kwenye mji mkuu Juba, Bwana Mogae ambaye ni rais mstaafu wa Botswana ametaka wale wote wanaohusika na vitendo hivyo wafikishwe mbele ya sheria.

Hata hivyo amesema uwajibikaji kisheria katika masuala hayo unatiwa doa na kutokuwapo kwa mahakama ya ngazi ya juu.

(Sauti ya Mogae)

“Hakuna maendeleo yoyote juu ya kuanzishwa kwa mifumo na taasisi kwa mujibu wa sura ya Tano ya makubaliano ya amani. Sijasikia lolote kutoka Muungano wa Afrika kuhusu kuanzishwa kwa mahakama ya ngazi ya juu kuhusu Sudan Kusini.”

Bwana Mogae amesema kwa kuzingatia mzozo unavyozidi kushika kasi Sudan Kusini, utekelezaji wa ibara hiyo ya tano ni muhimu zaidi hivi sasa na ametoa wito kwa pande zote kuimarisha jitihada zao ili iweze kutekelezwa.

Ameeleza pia masikitiko yake kuwa jopo lililotumwa kwenda kuchunguza ghasia za mwezi uliopita huko Wau Shilluk, mara kwa mara lilizuiliwa na vikosi vya SPLA upande wa serikali akisema hatua hiyo ni kinyume na makubaliano.

Sura ya tano ya mkataba wa amani wa Sudan Kusini inazungumzia kipindi cha mpito cha haki, uwajibikaji wa makosa na maridhiano ikiwamo kuundwa kwa tume ya maridhiano na mahakama ya haki.