Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Imarisheni sitisho la mapigano Syria tufikie walengwa- Guterres

Imarisheni sitisho la mapigano Syria tufikie walengwa- Guterres

Kwa miaka sita sasa, wananchi wa Syria wamekuwa wahanga wa moja ya majanga makubwa zaidi kukumba dunia zama za sasa.

Ndivyo ilivyoanza taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António  Guterres aliyoitoa wakati huu ambapo vita hivyo vinaingia mwaka wa saba ambapo ametangaza maombi mawili ya dharura.

Mosi ametaka pande husika kutumia ipasavyo sitisho la mapigano la tarehe 30 mwezi Disemba mwaka jana lililotangazwa na wahisani wa mazungumzo ya Astana.

Ametaka sitisho hilo liimarishwe ili kuhakiksiha misaada ya binadamu inafikia wahusika bila vikwazo vyovyote.

Ombi la pili ameelekeza kwa wale wote wenye ushawishi na pande husika kwenye mzozo wa Syria ili ziweze kumaliza tofauti zao na hivyo kufanikisha mazungumzo baina  yao huko Geneva.

Amesema msingi wa mazungumzo hayo ni  taarifa ya pamoja ya Geneva na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo lile namba 2254.

Katibu Mkuu amesema kupatikana amani nchini Syria ni jambo muhimu kimaadili na kisiasa na hivyo haiwezi kusubiri.

image
Baba akiwa na mwanae ndani ya meli moja ya kiitaliano baada ya kuokolewa kwenye bahari ya Mediteranea wakiwa safarini kutoka Syria kwenda Ulaya kusaka hifadhi. (Picha: UNHCR/A. D’Amato)
Naye msaidizi wa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada  ya dharura, Stephen O’Brien amesema machungu waliyoshuhudia wananchi wa Syria kwa miaka sita nchi yao ikisambaratishwa hayapaswi kuendelea.

(Sauti ya O’Brien)

“Tunaungana na waSyria tukitumai kuwa mwaka 2017 janga litakwisha. Mwaka ambao pande kwenye mzozo na wale wanaounga mkono vitendo vyao watarejesha hisia zao za kibinadamu. Mwaka ambao vizuizi kwenye maeneo vinaondolewa na misaada ya kuokoa maisha inapitishwa bila vikwazo na kufikia wahitaji. Mwaka ambao mashambulizi dhidi ya hospitali yanakoma na badala yake kunakuwa na fursa ya kujenga na vifaa vya matibabu vinapelekwa. Mwaka ambao maisha tena hayawekwi hatarini tena na watu wanaanza kazi ya kujimudu wakianza safari ndefu ya kujikwamua.”

Wakati huo huo, shirika la afya duniani, WHO limesema baada ya miaka sita ya vita nchini Syria, nusu ya hospitali nchini humo ndio zinaweza kutoa huduma.

Mkurugenzi Mtendaji wa WHO anayehusika na miradi ya afya ya dharura, Peter Salama amesema hata katika hospitali zilizo wazi, bado kuna uhaba wa maji safi na salama, umeme na vifaa vya kutosha vya matibabu.

Amesema hali hiyo inatokana na kwamba sitisho la mapigano linalokumbwa na utata bado halijawawezesha kufikia wananchi wanaohitaji huduma za afya.

Ametoa wito kwa pande kinzani nchini Syria kupatia ruhusa watoa huduma za kibinadamu ili waweze kufikisha maeneo husika vifaa vya matibabu ili kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji tiba.