Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yaanza kutoa chanjo dhidi ya Kipindupindu

Somalia yaanza kutoa chanjo dhidi ya Kipindupindu

Serikali ya Somalia kwa usaidizi wa shirika la afya duniani, WHO limeanza kutoka chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa watu zaidi ya 450,000 nchini humo.

Mwakilishi wa WHO nchini Somalia Dkt. Ghulam Popal amesema watoto wenye umri wa kuanzia miaka miwili hadi watu wazima watapatiwa chanjo hiyo ya matone kwa awamu mbili kwenye maeneo ya Mogadishu, Kismayo na Beledweyne ambayo yako hatarini zaidi.

Hii ni mara ya kwanza kwa aina hiyo ya chanjo kutolewa nchini Somalia wakati huu ambapo kipindupindu kimesababisha vifo vya watu 268 tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2017.

WHO imesema kampeni inafanyika wakati ambapo ukame umetangazwa kuwa ni janga la taifa na kuna uwezekano wa baa la njaa kukumba tena nchi hiyo.