Skip to main content

Watoto wa Syria na wimbo #Heartbeat wa kuibua matumaini

Watoto wa Syria na wimbo #Heartbeat wa kuibua matumaini

Miaka sita ya vita nchini Syria ikiwa imetimu, watoto nchini humo wameimba wimbo uitwao Heartbeat au mapigo ya moyo kwa lengo la kutuma ujumbe wa matumaini licha ya madhila wanayokumbana nayo kila uchao. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora)

Nats..

Wimbo unaanza kwa kuonyesha magofu yatokanayo  na mapigano ya miaka sita sasa nchini Syria.. huku kishada kikipeperuka kwenda hewani kuonyesha matumaini..

Nats..

Mwimbaji ni mtoto wa kike Ansam mwenye umri wa miaka 10 akiwa amevalia rinda lake maridadi anapaza sauti.. akisema katikati ya uharibifu na moto.. vidonda vyetu ni vikubwa ..tunataka kuzungumza lakini sauti zetu ni dhaifu..sisi tu watoto lakini kilio chetu kinatoka moyoni..tunataka kuondoa hofu..tunataka kuwa mabadiliko. Hebu mtu asikilize..tunataka utoto wetu!

Nats..

Akiwa amezaliwa na ulemavu wa kutoona, Ansam anaimba kibao hiki kilichotungwa na balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Zade Dirani.

Akishirikiana na watoto wengine 40 wa kike na wa kiume wanapaza sauti za matumaini wakisema nyoyo zetu zinadunda kwa ajili ya uhai na nyuso zetu zitang’ara.

Watoto hao ni miongoni mwa watoto milioni Tatu wanaoishi katika kambi za wakimbizi wa ndani nchini Syria, wakipatiwa huduma na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Akizungumzia kibao hicho,  mwakilishi wa UNICEF kanda hiyo Geert Cappeleare amesema ingawa sauti ya Ansam haiwezi kujenga upya magofu, bado kibao hicho kinaweza kuunganisha siyo tu wananchi wa Syria bali pia wakazi wengine duniani.