Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC yaanzisha mkakati mpya kupambana na mihadarati

UNODC yaanzisha mkakati mpya kupambana na mihadarati

Mkurugenzi mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya dawa na uhalifu UNODC Yury Fedotov akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha 60 cha tume inayohusika na dawa za kulevya CND mjini Vienna, Austria ameelezea juhudi za ofisi yake kukabiliana na tatizo la uhalifu wa dawa hizo na kusema wameanzisha mkakati uitwao maendeleo mbadala ili kuwalenga wanaofanya kilimo cha afyunyi, koka, kasumba, bangi na vingine ili kupunguza na kuboresha hali ya maisha ya wakulima kwenye maeneo magumu. Amesema kuwa UNODC pia inasaidia nchi kuwanasa wanaotekeleza uhalifu huo ili wawajibishwe.

Wanashirikiana na CND inayosimamia utungaji wa sera na masuala yanayohusiana na dawa za kulevya katika Umoja wa Mataifa. Bwana Fedotov amesema hivi karibuni, ofisi yake imeungana na Shirika la Afya Duniani WHO kutibu wanaotumia mihadarati kama njia mbadala ya kuwaadhibu.

Katibu Mkuu wa Umoja António Guterres akitoa ujumbe wake kwa njia ya video amesema juhudi za kupambana na dawa za kulevya zinaweza kusaidia kuendeleza maendeleo mapema na kufuta umaskini ikiwa ni sehemu yaajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.

Bwana Guterres ameongeza kuwa ana matumaini tume hiyo itapata mafanikio katika utekelezaji wa sheria, kuzuia, huduma za afya, haki za binadamu na maendeleo, akiongeza kuwa tume hiyo ina nafasi nzuri ya kuimarisha sera kuhusu dawa za kulevya kabla ya mkakati wa sasa kumalizika mwaka 2019.