Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazingira safi shuleni ni jukumu letu sote

Mazingira safi shuleni ni jukumu letu sote

Shirika lenye kukuza elimu ya msichana Sudan Kusini limejikita katika kutoa mafunzo kwa walimu 2,500 na zaidi nchini kote kwa lengo la kuboresha mazingira safi na kuwafunza wanafunzi kujisafi mashuleni.

Akihojiwa na Redio Miraya ya Umoja wa Mataifa nchini humo, Yolanda Elly, Mshauri wa Kijinsia wa shirika hilo amesema ingekuwa vigumu zaidi wao kutoa mafunzo kwa maelfu ya wanafunzi, hivyo shirika lake likapata wazo la kuwafunza walimu ambao watawafundisha wanafunzi kwa urahisi, kwani mafunzo haya huchukua muda na yanahitaji marejeo.

Amesema baadhi ya mambo wanayofundisha ni kupiga mswaki, kuoga, kutotema mate madarasani kujikinga na magonjwa kama kifua kikuu, jinsi ya kutupa taka, jinsi ya kuweka maliwato safi, na usafi wa wasichana wakati wa hedhi.

(Sauti ya Yolanda)

"Tunataka tuwe na mazingira safi, na kuwa na watoto wenye afya nzuri mashuleni, mtoto mwenye afya si lazima awe mtoto asiye mgonjwa,na kuhakikisha magonjwa hayazuii watoto kukosa kwenda shule, na kuzuia magonjwa yanayozuilika badala ya kuyapata."