Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya makataba wa amani , machafuko yafurusha maelfu Colombia-UNHCR

Licha ya makataba wa amani , machafuko yafurusha maelfu Colombia-UNHCR

Licha ya kusainiwa kwa mkataba wa amani baina ya serikali ya Colombia na kundi la upinzani liitwalo FARC, mwezi Novemba mwaka jana, machafuko nchini humo yanaendelea kufurusha maelfu ya watu, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Mapigano baina ya vikosi hivyo yamedumu kwa miaka 50.

UNHCR licha ya kutambua juhudi za kusaka amani na kuhakikisha haki za wahanga, shirika hilo limeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa kiwango cha wakimbizi.

Kwa mujibu wa takwimu za UNHCR, takribani asilimia 13 ya idadi ya watu nchini Colombia ambayo ni milioni 7.4 ni wakimbizi wa ndani. Wengi wa wanaothiriwa na machafuko ni watu wenye asili ya Afrika na jamii za watu wa asili.

William Spindler ni msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswisi.

( Sauti ya Spindler)

‘‘Tangu kusainiwa kwa mkataba wa amani, kumekuwepo na ongezeko la machafuko yanayotekelezwa na vikundi vipya vyenye silaha ambapo watu wengi wamefariki, wanatumikishwa kwa nguvu, wakiwamo watoto, ukatili wa kijinsia na ukosefu wa elimu, maji na huduma za usafi pamoja na kuzuiwa kutembea, na kufurushwa kwa raia. Tunasisitiza umuhimuwa raia kupatiwa ulinzi na usaidizi. Kadhalika, urejeshaji wa wakimbizi wa ndani katika maeneo yao ya asili ufanyike kwa usalama na utu.’’