Msaada wa chakula wawafikia maelfu ya wahitaji Sudan Kusini
Zaidi ya watu Laki Tatu waliokuwa wanakabiliwa na njaa huko Sudan Kusini wamefikishiwa misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula.
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu Jens Laerke amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kutangazwa kwa baa la njaa lililotokana na ukame kwenye maeneo ya Leer na Mayendit tarehe 20 mwezi uliopita.
(Sauti ya Jens)
“Mashirika ya kibinadamu nchini Sudan Kusini sasa wanajumuisha timu za za kufikisha misaada haraka kwa watu walioko maeneo yaliyoathirika zaidi na wameimarisha usambazaji wa vyakula, misaada ya dharura ya kuokoa maisha, virutubisho, huduma za afya na maji, usafi wa mazingira na huduma za usafi."
Hata hivyo amesema bado kuna karibu watu 100,000 wanaokabiliwa na baa la njaa na wale walio kwenye maeneo ya jirani Panyijiar Koch wako hatarini zaidi.
Fedha zaidi zinahitajika ili kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu nchini Sudan Kusini ambapo hadi sasa ni asilimia 9.3 ya dola bilioni 1.6 zilizoombwa mwaka jana ndio zimepatikana.