Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lalaani urushwaji wa makombora wa DPRK

Baraza la usalama lalaani urushwaji wa makombora wa DPRK

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha faragha hivi leo na kupokea taarifa ya mkuu wa Idara ya maswala ya kisiasa Jeffrey Feltman kufuatia hatua ya hivi karibuni cha Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK kurusha makombora manne ya masafa marefu. Makombora matatu kati ya hayo yalitua baharini kwenye ukanda wa kiuchumi wa Japan.

Baada ya kikao hicho, rais wa baraza hilo kwa mwezi wa Machi ambaye ni mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Matthew Rycroft akizungumza na wandishi wa habari amesema..

(Sauti ya Balozi Rycroft)

Kwanza kabisa tumelaani urushwaji wa makombora mnamo Machi 5 na DPRK, tukio hilo linaleta wasiwasi kwenye kanda. Ni lazima maazimio yaliyopitishwa ya baraza kuzingatiwa ili hatimaye kupata suluhu ya amani na kufuatilia kwa karibu masuala hayo. Pia tumepitisha jukumu maalum kwa katibu mkuu kwa ajili ya kufuatiolia suala hili kama tulivyokubaliana kwenye mkutano wetu hapo jana.

Wakati huo huo mabalozi watatu kutoka Marekani, Japan na Korea ya kusini pia walitoa kauli zao. Balozi Nikki Haley wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa akizungumzia juu urushaji wa makombora hayo amesema ...

(Sauti ya Balozi Haley)

Kinachotutatiza ni kwamba lilitua baharini kwenye umbali wa maili 200 mwa  kutoka Japan na nia yao ilikuwa kufikia kwenye vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Japan. Hatuwezi kulichukulia kirahisi. Jumuiya ya kimataifa lazima ielewa kuwa kila nchi iko mashakani kwa hatua hii ya Korea ya kaskazini na kila nchi inahitajika kuchukua hatua kukabiliana na  tishio hilo la  Korea ya kaskazini.

Naye mwakilishi wa Japan kwenye Umoja wa Mataifa Koro Bessho akasema

(Sauti ya Balozi Bessho)

Hii ni hatari kubwa kwa kuwa makombora hayo matatu yalitua kwenye ukanda wa kiuchumi ambako wavuvi wetu wanfanya kazi yao ya kawaida. Napenda kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msimamo wao kwa ajili ya tishio la DPRK na nashukuru kuwa wanachama wa baraza wate wamelaani vikali juu ya shambulizi hilo.