Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majanga ya kimya kimya yanayosambaratisha mazao mara nyingi hupuuzwa: FAO

Majanga ya kimya kimya yanayosambaratisha mazao mara nyingi hupuuzwa: FAO

Linapokuja suala la kulinda mazao na maisha ya kilimo, majanga ya kimyakimya mara nyingi hayaripotiwi na yanaweza kutokea mara nyingi na kufanya uharibifu mkubwa kuliko kimbunga au mafuriko.

Hayo yamesemwa na Anna Ricoy, afisa wa shirika la chakula na kilimo FAO katika kanda ya Amerika ya Kusini ambaye ni mtaalamu wa hatari ya majanga.

Bi Ricoy ameyasema hayo baada ya kikao cha ngazi ya juu kuhusu ujenzi wa uhimili wa majanga kwenye mkutano wa tano wa upunguzaji hatari ya majanga kwa mataifa ya Amerika unaofanyika Montreal, Canada.

Bi Ricoy, amesema utafiti wa kimataifa wa FAO unaonyesha kwamba asilimia 80 ya athari kubwa za ukame zinabebwa na sekta ya kilimo

(SAUTI YA ANNA RICOY)

“Asilimia 22 ya hasara zinazosababishwa na majanga ya wastani au makubwa , katika nchi zinazoendelea zinabebwa na sekta ya kilimo katika kiwango cha kimataifa. Na katika ukulima wa ngazi ya familia kwa wakulima wadogowadogo athari za majanga zinauweka uhakika wao wa chakula njia panda, sio tu kwamba wanapoteza kwa muda kipato au mazao yao lakini pia uhakika wao wa chakula unakuwa hatarini kwa sababu wanaishi kwa kutegemea kilimo”