Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitakubali anayepeperusha bendera ya UM atutie aibu- Guterres

Sitakubali anayepeperusha bendera ya UM atutie aibu- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewasilisha ripoti yake mbele ya Baraza Kuu inayotaja mikakati mipya mahsusi ya kuepusha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kingono kwenye operesheni za ulinzi wa amani za chombo hicho.

Amesema mikakati hiyo ni muhimu kuhakikisha hakuna mtuhumiwa yeyote anakwepa sheria wakati huu ambapo watuhumiwa wa vitendo hivyo mwaka jana pekee ni 145, ambapo 80 kati yao ni walinda amani askari na polisi huku 65 wakiwa ni wafanyakazi wa kiraia wa Umoja wa Mataifa.

Guterres amesema hatokubali mtu yeyote anayefanya kazi akiwa na bendera ya Umoja wa Mataifa kutekeleza au kutetea ukatili huo wa kingono hivyo mikakati yake ni ..

(Sauti ya Guterres)

“Mosi kuweka mbele haki na utu wa wahanga. Pili kujikita katika kukomesha ukwepaji sheria kwa waliokutwa na hatia ya uhalifu na unyanyasaji. Tatu, kutumia hekima na muongozo wa waathirika, asasi za kiraia, jamii na wengine kuimarisha na kuboresha juhudi zetu. Nne hatimaye, kuelimisha na kubadilishana uzoefu ili kumaliza janga hili.”

Mathalani katika kuweka mbele utu wa wahanga, Katibu Mkuu amepanga kukutana nao na kuwaelezea hatua mahsusi zinazochukuliwa na pia atateua msaidizi wake atakayehusika na utetezi wa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kingono.

Kuhusu kushirikisha nchi wanachama, Guterres amesema kando mwa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu, ataitisha kikao cha ngazi ya juu kujadili ukatili wa kingono na unyanyasaji.

Na hatimaye amesema.

(Sauti ya Guterres)

“Tutangaze kwa sauti moja: Sisi hatutomvumilia mtu yeyote atakayefanya au kuruhusu ukatili wa kingono na unyanyasaji. Hatutoruhusu mtu yeyote kuficha uhalifu huu na bendera ya Umoja wa Mataifa. Kila muathirika anastahili haki na msaada wetu. Kwa pamoja na tutimize ahadi hii.”