Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMA yalaani shambulizi kwenye hospitali mjini Kabul

UNAMA yalaani shambulizi kwenye hospitali mjini Kabul

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA umelaani shambulizi la kigaidi lenye utata lililotekelezwa mjini Kabul  asubuhi ya kuamkia hivi leo ambako wahusika waliovalia mavazi ya daktari walilipua gari la kujitoa mhanga katika mlango wa hospitali  ya Sardar Mohammad Daud Khan na kusababisha vifo na majeruhi ambapo, idadi kamili bado haijulikani.

Naibu mkuu wa UNAMA, Pernille Kardel amesema shambulizi hilo ni la kinyama kuwalenga watu katika mazingira magumu zaidi, wakati wanapata tiba hospitalini, na pia kuwalenga wafanyakazi. Ameongeza kuwa ukatili huo haukubaliki na lazima wahusika wawajibishwe. Hospitali hiyo ni mmoja ya hospitali kubwa nchini Afghanistan na huwatibu wagonjwa wa vikosi vya jeshi na familia zao.

UNAMA imesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya hospitali, mauaji au kudhulumu watu kwa makusudi ikiwa ni pamoja na wagonjwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa ambao ni uhalifu wa kivita. Ujumbe huo umezitaka pande zote katika mgogoro kuheshimu na kulinda wafanyikazi wote wa huduma za afya katika kufuata sheria za kimataifa. Bi Kardel ametuma rambirambi zake kwa familia za waliouawa na kuwatakia nafuu ya haraka kwa wale waliojeruhiwa.