Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuisha sauti za wanawake kwenye mchakato amani Maziwa Makuu- Djinnit

Jumuisha sauti za wanawake kwenye mchakato amani Maziwa Makuu- Djinnit

Kujumuisha wanawake katika mchakato wa amani kwenye ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika ni muhimu kwa kuwa inaleta maslahi mengi na endelevu kwa jamii na mataifa kwa ujumla.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye ukanda huo Said Djinnit ametoa wito huo leo ikiwa ni siku ya wanawake duniani akisema ili kuondoa mzizi wa mzozo unaoendelea Maziwa Makuu na kurejesha amani endelevu, ni lazima sauti za wanawake na wasichana zisikilizwe.

Kwa mantiki hiyo ametaka wadau wa amani wahakikishe wanawake wanashiriki ipasavyo kwenye mkataba wa amani, usalama na ushirikiano uliotiwa saini miaka mitatu iliyopita.

Bwana Djinnit amesema kwa upande wake yeye amesalia na azma yake ya kutetea ushiriki kamilifu wa wanawake na wasichana ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya wakazi wa ukanda huo wa maziwa makuu.