Skip to main content

Dola Bilioni 2 zahitajika kusaidia Kenya, Ethiopia na Somalia: UM

Dola Bilioni 2 zahitajika kusaidia Kenya, Ethiopia na Somalia: UM

Zaidi ya dola bilioni 2 zinahitajika kwa ajili ya misaada ya kibinadamu nchini Kenya, Somalia na Ethiopia mwaka huu wa 2017.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya naibu wa msemaji wa ofisi ya masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Jens Laerke.

Kwa upande wa Somalia pekee msemaji huo amekaribisha mchango wa dola milioni 100 ambazo tayari zimepokelewa huku fedha zaidi zikiahidiwa kutokana na ombi la dola milioni 825 lililozinduliwa na mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu mnamo Februari 18.

(Sauti ya Laerke) 

"Tunafahamu kuwa tukichukua hatua mapema kama hivi leo na fedha za wahisani kupatikana kwa haraka na kufanya kazi kwa pamoja tunaweza kubadilisha mwenendo huo ili isiwe janga. Tunaweza kubadilisha taswira ili tusianze kuona picha za watu waliobaki mifupa pekee." 

Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni 6 na nusu wanahitaji msaada na karibu milioni tatu kati yao hawawezi kukidhi mahitaji yao ya kila siku ya chakula.

Halikadhalika takribani watu 185,000 wanahitaji matibabu ya haraka huku visa vya kuhara na kipindupindu vikiripotiwa kuongezeka nchini Somalia.