Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amerika himizeni kujihami na majanga: UM

Amerika himizeni kujihami na majanga: UM

Majanga kama vile kimbunga Matthew yaliyokumba bara Amerika miaka ya hivi karibuni, ni udhihirisho wa changamoto zinazokabili dunia katika kufikia malengo ya mkataba wa Sendai wa kupunguza majanga.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza majanga UNISDR Robert Glasser amesema hayo hii leo wakati akifungua mkutano wa tano kuhusu kupunguza majanga barani Amerika unaoendelea nchini Canada.

Mkataba wa Sendai uliokubaliwa na nchi wanachama 187 mwaka 2015 ulilenga kupunguza vifo na majeruhi kwa kubadilika kutoka kuhimili majanga hadi kuhimili hatari za majanga na kujiandaa vyema.

Bwana Glasser amesema bado mwamko wa kukabiliana na majanga katika ukanda huo ni mdogo akitolea mfano wa kimbunga Matthew ambapo amesema matukio kama hayo yanatarajiwa zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kimbunga Matthew kilisababisha vifo vya zaidi ya raia wa Haiti 500 na kusababaisha hasara ya dola bilioni 2.78.