Skip to main content

Mipango ya Hungary kuwashikilia waomba hifadhi yatia hofu:UNHCR

Mipango ya Hungary kuwashikilia waomba hifadhi yatia hofu:UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatiwa hofu na sheria mpya iliyopigiwa kura jumanne kwenye bunge la Hungary ambayo itafanya kuwa lazima kuwashikilia waomba hifadhi wote wakiwemo watoto kwa kipindi chote cha mchakato wa kuomba hifadhi.

Kwa mujibu wa UNHCR hii inamaanisha kwamba kila muomba hifadhi wakiwemo watoto watazuiliwa kwenye makontena yaliyozingirwa na uzio wa waya mpakani katika kipindi kirefu, na hilo halikubaliki , kwani sheria hiyo mpya inakiuka wajibu wa Hungary chini ya sheria za kimataifa na za Muungano wa Ulaya. Cecile Pouilly ni msemaji wa UNHCR

(SAUTI CECILE POUILLY)

"Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na za Muungano wa Ulaya, kuwashikilia wasaka hifadhi kunaweza kuhalalishwa katika mazingira mahsusi na wakati kuna uhitaji na njia mbadala zinapaswa kuzingatiwa kwanza. Kukiuka hilo ni kitendo holela kwani watoto hawapaswi kuzuiliwa  kwa mazingira yoyote yale kwani hiyo haiendani na maslahi ya mtoto."