Mzizi wa ubaguzi wa wanawake bado unamea- Wataalamu
Harakati za kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake zimeendelea kugonga mwamba licha ya mafanikio katika baadhi ya maeneo tangu kuanza kwa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani zaidi ya karne moja iliyopita.
Hiyo ni kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wanawake waliokutana leo huko Geneva, Uswisi kuangazia siku ya wanawake itakayoadhimisha tarehe 08 Machi.
Wamesema mizizi ya ubaguzi wa kijamii, kisiasa na kiuchumi bado haujang’olewa wakitolea mfano baadhi ya maeneo ambako sheria za familia au ajira zinazuia fursa za wanawake katika nyanja mbali mbali.
Kwa mantiki hiyo wamezitaka serikali kupatia suala la haki za wanawake kipaumbele cha juu katika mikakati yao ikiwemo vipaumbele vyao vya kisiasa.