Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viuatilifu vinatishia haki za binadamu- Wataalamu

Viuatilifu vinatishia haki za binadamu- Wataalamu

Wataalamu wawili maalum wa Umoja wa Mataifa wametaka kuwepo kwa mkataba mpya wa kimataifa utakaodhibiti na kuondokana na viuatilifu au madawa hatari yanayotumika mashambani.

Wataalamu hao Hilal Ever wa haki za chakula na Baskut Tuncak anayeangazia masuala ya sumu wamelieleza Baraza la haki za binadamu huko Geneva, Uswisi kuwa matumizi kupita kiasi ya viuatilifu kwa muktadha wa hakikisho la upatikanaji wa chakula, yamekuwa mwiba kwa afya ya binadamu na mazingira.

Mathalani wamesema viuatilifu husalia kwa muda mrefu kwenye ardhi na kuathiri mazao yanayopandwa na hatimaye kusalia kwenye chakula na sasa vinahusishwa na magonjwa kama vile saratani, vifo vya watoto na vingine vikihusishwa na kupungua kwa uzalishaji wa nyuki.

Kwa mantiki hiyo wametaka mkataba mahsusi wa kufuatilia mzunguko wa madawa hayo il kuondoa pengo la sasa la kulinda haki za binadamu na matumizi ya viuatilifu.