Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Niko Somalia kuonyesha mshikamano wangu:Guterres

Niko Somalia kuonyesha mshikamano wangu:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa António Guterres yuko ziarani nchini Somalia, akizuru Moghadishu na Baidoa kwa mara ya kwanza akiwa katika wadhifa huo ili kuonyesha mshikamano na watu wa taifa hilo ambao amesema wako katika hali ya madhila lakini pia matumaini. Flora Nducha na taarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Amesema wako katika madhila kutokana na vita na baa la njaa linalonukia nchini humo na mataifa mengine matatu ya Sudan kusini, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na Yemen ambako mamilioni ya watu wanahitaji msaada.

Akaongeza kuwa hata hivyo huu ni wakati pia wa matumaini

(SAUTI GUTERRES)

“Wakati wa matumaini kwa sababu Somalia inapindua ukurasa, rais mpya alichaguliwa, waziri mkuu mpya aliteuliwa, na kuna ari ya nguvu ya kuimarisha usalama na wakati huohuo kuboresha uwezo wa serikali kuanza kutoa huduma kwa watu, bila shaka ikihitaji mshikamano wa jumuiya ya kimataifa.”

Leo hii kuna watu zaidi ya milioni sita Somalia wanaohitaji msaada, huku watoto zaidi ya laki tatu wakiwa na utapia mlo uliokithiri, na Guterres amesema bila msaada unaohitajika basi itakuwa zahma kubwa iliyokubalika na watu wa Somalia hawastahili hayo.