Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

EU yapigia chepuo mlo shuleni nchini Burundi

EU yapigia chepuo mlo shuleni nchini Burundi

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limekaribisha msaada wa zaidi ya dola milioni Tano kutoka Muungano wa Ulaya, EU kwa ajili ya mradi wa mlo shuleni nchini Burundi.

Mwakilishi mkazi wa WFP nchini Burundi Charles Vincent amesema fedha hizo zitaelekezwa jimbo la Gitega, katikati mwa nchi ambako siyo tu zitaimarisha uwezo wa watoto shuleni, bali pia kuinua uhakika uzalishaji wa kilimo na kuepusha utapiamlo.

Amesema watanunua chakula kutoka wa wafanyabiashara Gitega na kusambaza shuleni ambako watoto watapatiwa mlo wa moto utokanao na wali, maharagwe na unga wa mahindi ulioongezewa virutubisho nchini humo.

Bwana Vincent amesema kwa kununua vyakula hivyo pamoja na maziwa ya ng’ombe kutoka kwa wakulima na wafugaji, WFP itakuwa inaongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa eneo hilo husika.

Nchini Burundi kiwango cha utapiamlo ni asilimia 58, hivyo WFP kupitia mradi wa mlo shuleni inalenga kuondokana na hali hiyo miongoni mwa watoto na wajawazito 20,000 na wakati huo huo kuchochea watoto kwenda shuleni.