Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita dhidi ya boko haram viende sanjari na maendeleo endelevu

Vita dhidi ya boko haram viende sanjari na maendeleo endelevu

Wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakiwa wanaendelea na ziara yao katika bonde la ziwa Chad hivi leo jumapili wamekua nchini Niger kwa mara ya kwanza. Niger ni moja ya nchi maskini zaidi duniani.

Balozi Matthew Rycroft wa Uingereza ambaye ni rais wa baraza hilo mwezi huu wa Machi na pia kiongozi wa msafara huo akizungumza na wandishi wa habari katika mji mkuu Niamey ameahidi mshikamano na watu wa nchi hiyo.  Amesema kuwa dhamira yao ni kusaidia zaidi Niger katika jitihada zake za kurejesha utulivu na usalama katika maeneo ya bonde la ziwa Chad na kuhakikisha ulinzi na msaada kwa walioathirika na mgogoro.

Mapema wanachama hao walikutana na Rais Mahamadou Issoufou.

Wanachama hao pia walifanya mkutano na mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika kuhusu "hali mbaya" katika mkoa wa Diffa unaopakana na Nigeria ambako maelfu ya watu walikimbia kutokana na machafuko ya kikundi cha kigaidi cha Boko Haram. Mbali na ukosefu wa usalama, Niger inakabiliwa na ukame, jangwa na ukosefu wa ajira na shule kwa watu na vijana ambao ni theluthi mbili ya idadi ya watu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mpango wa maendeleo inasema kuwa Niger inashikilia nafasi 188 katika orodha ya maendeleo.

Akizungumza na wanachama hao mwakilishi mkazi wa UNDP na mratibu Fodé Ndiaye, amesema waathirika wanaishi na wenyeji wao na jamii nyingine duni zilizo pia kwenye mazingira magumu.

Balozi Rycroft amesema kuwa moja ya suala waliloshuhudia ni umuhimu wa lengo nambari 16 la maendeleo endelevu ambalo ni  kutetea amani na umoja kwa jamii, kutoa upatikanaji wa haki kwa wote na kujenga ufanisi na taasisi za umoja katika ngazi zote. Ameongeza kuwa kutembelea bonde la ziwa Chad wameona thamani ya lengo hilo.

Wanachama hao wanaelekea mjini Maiduguri, Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria ambao tangu 2009 kunajulikana kama kitovu cha uasi cha Boko Haram. Wakiwa huko watakutana na viongozi wa mitaa na asasi za kiraia na pia kutembelea kambi ya wakimbizi wa ndani. Watamalizia katika mji mkuu Abuja ambapo watakutana na kaimu Rais wa Nigeria Yemi Osinbajo.