Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 7 wanakumbwa na baa la njaa bonde la ziwa Chad:UM

Zaidi ya watu milioni 7 wanakumbwa na baa la njaa bonde la ziwa Chad:UM

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo liko nchini Chad ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya nchi nne kuangazia changamoto zinaoendelea za kibinadamu katika eneo la bonde la ziwa Chad  na kuongeza uelewa wa kimataifa kwa hatma ya watu wapatao milioni 11.

Ujumbe wa baraza hilo ukiwa katika mji mkuu N'Djamena umekutana na waziri mkuu Albert Pahimi Padacké na pia kutembelea kikosi cha pamoja cha askari kutoka nchi nne zilizoathirika kwenye kanda hiyo ikiwemo Cameroon, Chad, Niger na Nigeria, pamoja Benin wanakokabiliana na mapambano dhidi ya Boko Haram.

Majadiliano na Waziri Mkuu yalilenga hali ya kiuchumi nchini humo na umuhimu wa kuingiza wanawake katika masuala ya uchumi na kisiasa. Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Matthew Rycroft ambaye ndiye rais wa mwezi huu wa Machi wa Baraza la Usalama na kiongozi wa ziara hiyo amesema

(Sauti ya Rycroft) 

Sababu zilizotufikisha hapa ni kwamba hatutaki janga hili kusahaulika na ulimwengu, tungependa jumuiya ya kimataifa kuelewa hivyo. Pia tunataka kufanya kila juhudi kubaini kinachoendelea halafu tukirudi New York muda si mrefu tuweze kufahamu ni nini tunahitajika kufanya.”

Wanachama hao pia wamekutana na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi nchini Chad.  Wamegusia changamoto walizonazo katika kutoa misaada kwa mamilioni ya watu, kukabiliwa na uhaba wa chakula na lishe na migogoro iliyowafungisha virago watu milioni 2.4 na zaidi ya milioni 7.1 wanakumbwa na baa la njaa .

Katika mazungumzo yake na ujumbe wa Baraza la Usalama , mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo  Stephen Tool amesema nchi hizo zina changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na utapiamlo, magonjwa, na usafi wa mazingira. Amebainisha kuwa masuala ya kibinadamu hayawezi kushughulikiwa bila kuangalia mzizi ya sababu kama vile ukosefu wa usalama, mapengo ya maendeleo, ukosefu wa elimu, kilimo duni, na mengine.

Hapo jana Ijumaa timu hiyo ilitembelea Cameroon ambapo walikutana na Rais Paul Biya na maafisa wengine waandamizi wa Serikali. Na pia kukutana na watu waliokimbia  uasi wa Boko Haram. Ujumbe huo utaelekea Niger baadaye leo na kuzuru Nigeria hapo kesho jumapili.