Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wa jamii za asili Australia wakabiliwa na ukatili mkubwa:UM

Wanawake wa jamii za asili Australia wakabiliwa na ukatili mkubwa:UM

Mifumo mkingi ya ubaguzi imechochea kiwango kikubwa cha ukatili unaowakabili wanawake kutoka jamii za watu wa asili nchini austarlia. Hayo ni kwa mujibu wa mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake Dubravka Šimonović .

Bi Šimonović ambaye amekamilisha ziara nchini humo amesema wanawake wengi wanabaguliwa kimaumbile na kukabiliwa na ubaguzi wa rangi , lakini pia wanakumbwa na ubaguzi mwingine wa wa kuwekwa daraja la chini katika jamii kwa sababu ya hali yao ndogo kiuchumi.

Akiwa Australia mwakilishi huyo alipata fursa ya kukutana na wanawake wenye ulemavu na walio kifungoni kwenye magereza mbalimbali.

Ameongeza kuwa jamii za wanawake hao wa kabila la Aboriginal na wa kisiwa cha Torres Strait wametengwa na hawajumuishwi katika sera za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.