Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyongeza ya dola milioni 130 kusaidia miundombinu Tanzania- Benki ya dunia

Nyongeza ya dola milioni 130 kusaidia miundombinu Tanzania- Benki ya dunia

Benki ya dunia imeidhinisha nyongeza ya dola milioni 130 kwa ajili ya mradi wa Tanzania wa kuboresha miji, TSCP kupitia uimarishaji wa miundombinu.

Miji itakayonufaika ni Tanga, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Mbeya na Mtwara na lengo ni kuwezesha miji hiyo kuendana na kasi ukuaji wa miji.

Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Malawi, Somalia na Burundi, Bella Bird  amesema uboreshaji wa huduma katika miji hiyo ni muhimu ili kusaidia azma ya serikali ya kufikia lengo la kuwa nchi ya viwanda.

Amesema miji ina fursa kubwa ya kuimarisha maendeleo ya kikanda, kuunganisha watu kupitia masoko na kuchochea ukuaji wa viwanda nchini kote.

Mradi wa TSCP nchini Tanzania umekuwa unatekelezwa tangu mwaka 2010 ukilenga miundombinu mijini, kuimarisha taasisi na usaidizi katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Tangu kuanza kwake barabara zenye urefu wa kilometa 141 mijini zimejengwa, mitaro mikubwa kilometa 15 na vituo sita vya mabasi ikinufaisha watu zaidi ya milioni 1.2.