Vikosi vya serikali vimekiuka haki za binadamu DRC: UM

1 Machi 2017

Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC vilitumia nguvu kupita kiasi, isiyohitajika na hata silaha ili kudhibiti maandamano mwezi desemba mwaka 2016 , imebaini ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa Jumatano.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO ijulikanayo kama (UNJHRO), angalau watu 40 wakiwemo wanawake watano na watoto wawili waliuawa kati ya Desemba 15 na 31 mwaka 2016, katika miji mbalimbali ya DRC ikiwemo Kinshasa, Lubumbashi, Boma na  Matadi.

Ripoti hiyo imebaini kwamba watu 28 waliuawa na wanajeshi wa kikosi cha serikali (FARDC), sita waliuawa na wakala wa polisi wa taifa (PNC) na sita waliosalia waliuawa wakati wa operesheni ya pamoja ya PNC na FARDC.

Wote isipokuwa wawili waliuawa kwa risasi, huku watu wengine 147 wakijeruhiwa na 917 kukamatwa na kuwekwa ndani.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein ameitaka serikali ya DRC kuhakikisha kwamba wote waliohusika wanawajibishwa lakini pia serikali hiyo ipitishe mara moja sheria ya uhuru wa kuandamana kwa amani na inayowalinda watetezi wa haki za binadamu.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter