Hatutashinda kwa kubagua wengine- UNAIDS

1 Machi 2017

Leo ni siku ya kimataifa ya kupinga aina zote za ubaguzi ambapo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Ukimwi, UNAIDS limesema maudhi ya mwaka huu yanasihi kila mtu apaze sauti ili kupinga ubaguzi wa aina mbalimbali ikiwemo dhidi ya watu wenye virusi vya Ukimwi, VVU, au Ukimwi.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé amesema kutokubaguliwa ni  haki ya binadamu na hivyo ni vyema sheria na kanuni na mazingira bora vikawepo ili kundi hilo lipate matibabu bila vikwazo vyovyote.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa Bwana Sidibé amesema wanawake wenye VVU hawapatiwi huduma za afya ya uzazi hali inayosababisha wapate saratani ya mfuko wa uzazi ambao hatimaye hutolewa badala ya kupatiwa huduma, hivyo amesema…

(Sauti ya Sidibé)

“Nadhani hakikisheni watu wanaweza kuwasikia mkisema kuwa tunaweza kushinda, lakini kamwe hatutashinda kwa kubagua watu.”

Akaenda mbali kusema kile kinachokwamisha makundi kama vile wanaojidunga madawa ya kulevya, wapenzi wa jinsia moja kukosa huduma.

(Sauti ya Sidibé)

“Nadhani tunakabiliwa na tatizo kubwa la desturi na mila na vikwazo vya kitamaduni ambavyo tunapaswa kuondoa. Halikadhalika sheria na sera mbovu ambazo zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa cha kupata huduma.”

Tayari mwanamuziki  Adian Coker kutoka nchini Uingereza anapaza sauti kupinga ubaguzi kupitia kibao chake #ZeroDiscrimination.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter