Vikwazo dhidi ya silaha za kemikali Syria vyagonga mwamba

28 Februari 2017

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililolenga kuweka vikwazo kufuatia matumizi ya silaha za kemikali nchin Syria limegonga mwamba baada ya Urusi na China kupinga kwa kutumia kura zao turufu.

Azimio hilo lingalianzisha kamati na jopo la wataalamu ambao watawajibisha wale wote watakaotumia silaha hizo za kemikali kweney vita vya Syria vilivyoanza miaka sita iliyopita.

Ripoti ya pamoja ya shirika la Umoja wa Mataifa la kupinga matumizi ya nyuklia, OPCW na mfumo wa pamoja wa uchunguzi uliobaini kuwa serikali ya Syria na kikundi cha kigaidi cha ISIL walitumia silaha zilizopigwa marufuku pamoja na kikundi cha kigaidi cha ISIL.

Matthew Rycroft ni mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa na amezungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho cha leo cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokuwa kimekutana kujadili hali ya Syria na kupitisha azimio hilo.

(sauti ya Balozi Rycroft)

"Kwa kupigia kura turufu azimio la leo, wamekandamiza uhalali wa hili baraza na kanuni za kimataifa za kuzumia matumizi ya silaha hizi za kikatili. Hii haikuwa nyaraka ya kisiasa, ilikuwa ni nyaraka yenye azimio la kiufundi ikilenga kuchukua hatua kufuatia ripoti isiyoegemea upande wowote ya jopo lililopewa mamlaka na Baraza la Usalama. Ilikuwa ni ripoti ya kile tulichotaka.Ulikuwa ni uchunguzi ambao sote tuliunga mkono.”

Urusi ikieleza kwa nini imepinga azimio hilo, Naibu mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vladimir Safronkov amesema kuwa wamekuwa na shuku juu ya hitimisho la ripoti hiyo kuwa serikali ya Syria chini ya Rais Bashar Al Assad ilitumia silaha za kemikali.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter