Watu wa asili ya Afrika wananyanyasika na kubaguliwa Ujerumani:UM

Watu wa asili ya Afrika wananyanyasika na kubaguliwa Ujerumani:UM

Watu wenye asili ya Afrika nchini Ujerumani wanateseka na ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Waafrika, kuzongwa kwa sababu ya rangi yao katika maisha yao ya kila siku, lakini hali zao zinasalia mafichoni bila kuanikwa katika jamii, limesema jopo la wataalamu wa umoja wa Mataifa Jumatatu baada ya kuhitimisha ziara yao ya kwanza ya kikazi nchini humo.

Kitendo cha polisi nchini humo kuendelea kuwa katika hali ya kukana kwamba ubaguzi wa rangi upo Ujerumani na ukosefu chombo huru cha kufikisha malalamiko katika ngazi ya shirikisho na serikali kumezidisha ukwepaji sheria ameongeza Ricardo Sunga, kiongozi wa timu ya jopo hilo.

Kuanzia tarehe 20 hadi 27 februari ujumbe wa jopo hilo ulizuru ,Berlin, Dessau, Dresden, Frankfurt, Wiesbaden, Düsseldorf, Cologne na Hamburg ili kujionea na kupata uelewa kuhusu ubaguzi wa rangi , chuki dhidi ya waafrika, chuki dhidi ya wageni na vitendo vingine vya kutovumiliana vinavyowaathiri watu wa asili ya Afrika waishio Ujerumani.

Wataalamu hao wanaamini kwamba ubaguzi wa rangi wa kitaasisi katika mfumo wa haki nchini humo umesababisha kushindwa kuchunguza na kuwafungulia mashitaka wahusika wa ghasia za kibaguzi na uhalifu utokanao na chuki dhidi ya watu wenye asili ya Afrika.