Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama huko Kasai DRC yatia hofu Baraza la Usalama

Hali ya usalama huko Kasai DRC yatia hofu Baraza la Usalama

Ghasia katika miezi ya hivi karibuni kwenye jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC zimetia hofu kubwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe wa Baraza hilo wametoa taarifa yao wakisema wanatiwa hofu zaidi na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu za kimataifa ikiwemo wanamgambo kutumikisha watoto vitani na jeshi la serikali kuua raia.

Wamesema vitendo vyote hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa hivyo wametaka serikali iwajibike kulinda raia na ijizuie kutumia nguvu za kijeshi kupita kiasi.

Wameitaka serikali kufanya uchunguzi usioegemea upande wowote na wahusika wafikishwe mbele ya sheria huku wakisema kuwa ujumbe wa umoja huo DRC, MONUSCO utakuwa tayari kusaidia iwapo utaombwa kufanya hivyo.

Kuhusu uchaguzi, wajumbe hao wamesisitiza umuhimu wa serikali ya DRC na wadau wa kitaifa kuchukua hatua zote muhimu za kuandaa uchaguzi huo bila kuchelewa na kuhakikisha mazingira ni salama kwa uchaguzi huru na haki.

Wametoa wito kwa wadau wa maendeleo wa DRC kusaidia ili kufanikisha uchaguzi huku wakisema wako tayari kufanikisha utekelezaji wa makubaliano ya tarehe 31 mwezi Disemba mwaka jana yanayohusisha pia uchaguzi.